WIKI hii droo ya Nusu Fainali ya michuano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federations Cup (ASFC) 2016 imepangwa na vigogo Azam na Yanga wote watacheza ugenini.
Yanga SC watamenyana na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na Azam FC itamenyana na Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, mechi zote zikipigwa Aprili 24, mwaka huu.
Coastal Union iliingia Nusu Fainali baada ya kuitoa Simba SC kwa kuifunga mabao 2-1, wakati Azam FC iliitoa Prisons kwa kuifunga 3-1, Mwadui FC iliitoa Geita Gold kwa kufunga 3-0 na Yanga SC iliwafunga Ndanda FC 2-1.
Bingwa wa Kombe la ASFC, michuano iliyoanza na timu 64 Novemba mwaka jana, ataiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Katika hatua ya awali, kila timu ilipatiwa fedha za usafiri Sh Milioni 3, na vifaa vya mashindano kutoka kwa wadhamini, Azam TV ikiwa ni sehemu ya udhamini wa Bilioni 3.3.
Bingwa wa Kombe la ASFC atajinyakulia kitita cha Sh. Milioni 50, Fainali inatarajiwa kuchezwa wiki moja baada ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kumalizika mwezi ujao.
Mara ya mwisho michuano hiyo ilifanyika mwaka 2002 na JKT Ruvu ikaifunga Baker Rangers ya Magomeni katika fainali, wakati huo ikijulikana kama Kombe la FAT (Chama cha Soka Tanzania).
Moja kati ya mambo ya maana sana katika ustawi wa soka ya Tanzania yaliyofanyika chini ya uongozi wa Rais Jamal Malinzi TFF ni kurejesha michuano hiyo.
Michuano hii hairudi kama fasheni kwa sababu nchi nyingine zinafanya, hapana – bali imekuja kutoa fursa ya kufichua vipaji zaidi na pia kuwaongezea idadi ya mechi za kucheza kwa msimu wachezaji wa timu za Ligi Kuu, jambo ambalo litawaongezea pia uimara kimchezo.
Lakini pia, baada ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Agosti na Mei – kalenda ya msimu wa soka ya Tanzania imekuwa haina cha zaidi, jambo ambalo hakika kwa namna moja au nyingine limekuwa likitukwamisha sehemu bila wenyewe kujua.
Uganda ni nchi ambayo inaongoza kisoka katika ukada wetu wa Afrika Mashariki na Kati na hiyo inatokana na mambo kadhaa, kubwa ikiwa ni pamoja na kuwa mashindano mengi ya nyumbani.
Pamoja na Ligi Kuu ambayo pia inadhaminiwa na kampuni ya Azam, Uganda wana michuano ya Kombe la shirikisho lao (FUFA) na ligi ya wachezaji wa akiba.
Ndiyo maana kila siku Uganda imekuwa ikizalisha nyota ambao wanazitamanisha klabu za nchi nyingine za ukanda huu, zikiwemo za kwetu Tanzania.
TFF inastahili pongezi kwa kufanikisha kurejesha michuano hii – na pongezi zaidi kwa Azam ambao kwa sasa ni kati ya mihimili mikuu mitatu ya soka ya Tanzania upande wa uwezeshaji, mingine ikiwa ni Vodacom Tanzania wadhamini wa Ligi Kuu na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), wadhamini wa Taifa Stars, Simba na Yanga.
Pamoja na pongezi hizo kwa TFF na kwa wadhamini wa mashindano, Azam TV, nataka niainishe mambo machache ya kurekebisha ili kuyaongezea ladha na uzito stahili mashindano hayo.
Mfano ni mechi za Nusu Fainali kuchezwa katika Uwanja wa timu mojawapo, badala ya kuchezwa kwenye Uwanja ambao hauhusiani na timu yeyote baina ya zinazokutana.
Inavyoonekana kabisa TFF inaendesha Kombe la ASFC kwa kuiga mfumo wa Kombe la FA England – lakini kwa wenzetu hao mashindano yao yanapofikia hatua ya Nusu Fainali timu hukutana katika Uwanja ambao hauhusiani na timu yoyote miongoni mwa zinazokutana.
Na hiyo ni kujaribu kutengeneza haki kwa timu zinazokutana, kwani inaaminika kucheza nyumbani ni kipaumbele.
Naamini kwa mwaka huu wa kwanza tangu kurejea kwa michuano hiyo TFF haiwezi kubadili kitu katika mfumo wa mashindano.
Isipokuwa TFF inaweza kuchukua changamoto na mapungufu mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mashindano ya mwaka huu kwa ajili ya kuboresha mashindano ya mwakani.
Pamoja na hilo, lakini pia, baadhi ya viwanja ambavyo msimu huu vimetumika kwa ajili ya mashindano hayo vimekuwa havina sifa, mfano Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.
Sheria namba moja katika sheria 17 za soka ni; Eneo la kuchezea (The Field of Play), ambayo inasema soka lazima ichezwe katika Uwanja wa nyasi ama halisi, au za bandia, lakini mwonekano lazima uwe rangi ya kijani.
Eneo la kuchezea mpira linapaswa kuwa katika mwonekano mzuri, wenye kuonyesha alama zote nyeupe za kugawa maeneo ya Uwanja na magoli yote mawili.
Tulishuhudia mchezo kati ya wenyeji Panone FC na Azam FC ya Dar es Salaam iliyoshinda 2-1 hatua ya 16 Bora Kombe la ASFC ukichezwa kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, ambao sehemu kubwa ya eneo la kuchezwa halina nyasi na lina mabonde, halijanyooka.
Hata kabla ya kuanza kwa mchezo, tulijiuliza Uwanja ‘kipara’ wa Ushirika unaruhusiwa vipi kutumika si kwa mashindano makubwa kama Kombe la TFF, bali mashindano yoyote ya soka ya ngazi yoyote, hata Daraja la 10 kama lipo.
TFF na Azam TV wanastahili pongezi kwa kurejesha ASFC, lakini wanapaswa kuelekea mashindano ya mwakani, wajifunze kutokana na mapungufu ya mwaka huu, ili ‘madudu’ haya yasijirudie.
CHANZO: BINZUBERY
0 Comments