Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdalah Bulembo amemtaka waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa amwache Rais Magufuli aendelee kufanya kazi zake.
Bulembo anakuwa kiongozi wa pili wa CCM kumvaa Lowassa aliyekosoa utendaji wa Rais Magufuli wa kutumbua majipu wakati alipokutana na wanazuoni wa ndani na nje ya nje Alhamisi ya wiki hii, baada ya juzi msemaji wa CCM Christopher Ole Sendeka naye kumkosoa kuwa si kweli kwamba watumishi wa umma wanafukuzwa bila kusikilizwa.
Akizungumza mjini hapa jana na wanachama wenzake wakati wa maadhimisho ya miaka 61 ya Jumuiya hiyo yaliyofanyika kitaifa mkoani Morogoro, Bulembo alimtaka Lowassa kutekeleza ahadi yake ya kwenda Monduli kuchunga ng'ombe kama hatochaguliwa kuwa Rais.
"Kama yeye anasema kasi ya Magufuli ni ya muda au anakosea kutumbua majipu, basi tunamkumbusha kauli yake wakati akiongea na vyombo vya habari kuwa akishindwa urais atarudi kijijini kwake kuchunga ng'ombe, tunaomba aende akafanye kazi aliyoahidi. " Alisema Bulembo.
Alisema anashangazwa na Liwassa aliyekuwa mgombea urais mwaka jana kupitia Chadema chini ya mwamvuli wa UKAWA kusema ndani ya CCM kumejaa ufisadi wakati yeye ni fisadi namba moja.
Katika hatua nyingine, Bulembo alisema ndani ya CCM kuna majipu yanayohitaji kutumbuliwa wakiwemo Wasaliti.
Alisema wanasubiri Rais Magufuli akabidhiwe uenyekiti wa CCM mwezi wa saba mwaka huu ili waanze kuyatumbua majipu hayo.
0 Comments