Header Ads Widget

Ripoti Ya Polisi Kuhusu Tukio la Ujambazi Mbagala: Waliofariki Dunia ni Watu 7........Kati Yao Majambazi ni 3, Askari 2 na Raia 2




Ujambazi wa kutumia vifaa vya kivita umeibuka jijini Dar es Salaam, ukiwemo uliofanyika katika uporaji wa Benki ya Access juzi, ambako majambazi walitumia bunduki za kivita aina ya SMG na mabomu ya kurusha kwa mkono.


Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema mbali na uvamizi huo, pia Polisi imebaini na kukamata askari bandia, waliokuwa na sare rasmi za Jeshi la Polisi zenye vyeo na redio call, zenye uwezo wa kuingilia mawasiliano ya askari Polisi.


Akizungumzia matukio hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alisema atakutana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, ili Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi, waanzishe msako wa pamoja dhidi ya wahalifu hao.


Uvamizi, mauaji Mbagala
Akisimulia ujambazi uliofanyika katika Benki ya Access Tawi la Mbagala, Kamanda Sirro alisema majambazi hao walikuwa 12, wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki sita na walifika kwenye benki hiyo saa 8:30 mchana.


Baada ya kufika, moja kwa moja waliingia kwenye chumba cha askari wanaolinda benki na kumpiga risasi kichwani askari mwenye namba H7739 Konstebo Harid na kufa papo hapo.


Mbali na mauaji hayo, Kamanda Sirro alisema walimshambulia askari mwingine, Konstebo Shaban miguuni na kupora silaha zao na kuingia nazo ndani ya benki, ambako walimshambulia mlinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi na raia wengine wawili na kufa papo hapo, huku wengine watano wakijeruhiwa.


Baada ya hapo kwa mujibu wa Kamanda Sirro, majambazi hao walikimbilia chumba kinachohifadhi fedha nyingi (strong room) na kukipiga risasi katika jitihada ya kutaka kuingia ndani, lakini hawakuweza kuvunja.


Kutokana na ugumu wa kuvunja chumba hicho, Kamanda Sirro alisema haraka haraka wakahamia katika kaunta za watoa fedha na kupora fedha zilizokuwepo kati ya Sh milioni 20 mpaka Sh milioni 30 na kuondoka na silaha za polisi aina ya SMG mbili na ile yao moja pamoja na pikipiki zao.


Polisi waua watatu
Kamanda Sirro alisema taarifa zilisambazwa katika vikosi vya ulinzi, ambavyo vilijiimarisha.


Alitaja Kikosi cha Mbwa na Farasi eneo la Mkuranga, ambao walijiandaa na majambazi hao walipofika kijiji cha Chui wilayani Mkuranga mkoani Pwani, walipambana na polisi na askari wakafanikiwa kuua majambazi watatu.


Mbali na kuua watatu, silaha tatu zilikamatwa ambazo ndio zile SMG mbili za Polisi, walizochukua pamoja na ile yao moja, lakini wakakutwa pia na mabomu matatu ya kutupa kwa mkono yaliyotengenezwa Urusi.


“Hawa majambazi walikuwa wamejiandaa, kwa maana walikuwa na mabomu ya kutupwa kwa mkono matatu aina ya RGD 01 ambayo ni mbinu ya kujilinda wanaposhambulia,” alisema Kamanda Sirro.


Tisa watoroka
Pamoja na kujiimarisha kwa polisi, majambazi tisa walikimbia wakaacha pikipiki zote sita za aina tofauti, ambazo ni Haojue mbili zenye namba MC 560 AED na MC 207 BAN, San LG yenye namba MC 784 BDJ, Boxer yenye namba MC 248 AXE na King Lion mbili zenye namba MC 653 BDQ na MC 853 BDR.


Kamanda Siro alisema baada ya hapo, waliendelea kuwakimbiza majambazi hao hadi wakatokomea katika Msitu wa Kongowe, ambako juhudi za kuwatafuta zilianza mara moja.


“Nawahakikishia wananchi mtandao wote wa ujambazi kwenye mabenki na maeneo mengine, tutausafisha wote kwa maana hawa wanafanya uhalifu maeneo ya Dar es Salaam na Pwani na wana ndugu zao, tutawakamata wote,” alisisitiza Kamanda Sirro.


Alisema hawawezi kuona Watanzania wakiumia na kufa kwa tamaa za wachache, wenye kupenda utajiri wa haraka.


JWTZ kazini
Akizungumza kuhusu ujambazi huo, Waziri Kitwanga alisema Polisi inajipanga upya na atazungumza na Waziri mwenzake, Dk Mwinyi kuangalia jinsi ya majeshi hayo mawili, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), watakavyofanya kazi pamoja ya msako katika misitu yote inayozunguka mikoa ya Pwani, kuanzia Bagamoyo hadi Kisarawe.


Alionya kama kuna kambi za uhalifu ndani ya misitu hiyo, zitasambaratishwa na kuomba raia wema watoe taarifa za uhalifu.


“Tutafanya operesheni kubwa na tutaifanya haraka, tunaomba wananchi watoe ushirikiano hasa waendesha bodaboda kwa maana zinatumika sana kwenye matukio haya. Mtandao wa majambazi ufahamu kwamba vyombo vya usalama havijalala, tutawamaliza wote, tutatumia nguvu zetu zote kuwamaliza na tutafanikiwa,” alisisitiza Kitwanga.


Kuhusu waendesha bodaboda, Kitwanga alisema ukaguzi wa kina unafanywa na kuwataka waendesha bodaboda hao wanaposimamishwa, wakubali na kutoa ushirikiano na wasione kama wanabughudhiwa, bali ni kuwakagua kwa sababu wahalifu hutumia vyombo hivyo zaidi kufanya matukio mabaya.


Polisi feki
Katika tukio jingine, Kamanda Sirro alisema polisi feki wanne wamekamatwa na wanashikilia kwa mahojiano, ili kubaini mtandao huo ambao unatumia sare za Polisi, redio za upepo na pingu kufanya matukio ya uhalifu.


Alisema walipata taarifa kutoka kwa raia wema ya kuwepo kwa mtandao wa askari bandia, ambao hutumia sare za jeshi hilo kufanya matukio ya uhalifu, ndipo walipowakamata hao wanne.


Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, polisi feki watatu walikamatwa Februari 24, asubuhi saa mbili eneo la Upanga karibu na Daraja la Selander.


Alisema watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa, walikiri kufanya matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha na kumtaja mtuhumiwa mwenzao mmoja anayeishi Kinyerezi.


Kamanda Siro alisema Polisi walimfuata mtuhumiwa huyo nyumbani kwake Kinyerezi na walipofanya upekuzi, walimkuta na sare halisi ya Polisi, redio ya upepo na pingu.


Kamanda Sirro alisema baada ya uchunguzi, imebainika kwamba watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia sare na vifaa hivyo vya Polisi, kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi kwa kujiaminisha kuwa wao ni askari Polisi.


Alisema watuhumiwa hao wamekiri kufanya matukio mbalimbali, ikiwemo kuweka vizuizi katika barabara za mikoani na kufanya uporaji.


“Watuhumiwa hao wote wanahojiwa ili waeleze jinsi walivyopata sare na vifaa hivyo ya Polisi, wamekiri kufanya uhalifu maeneo mbalimbali, lakini wakati mwingine tunashindwa kukamata wahalifu kwa sababu redio call wanayotumia zinaingiliana na zetu, hivyo wanakuwa wamepata taarifa,” alisema Kamanda Sirro.


Katika tukio lingine, Februari 18 mwaka huu, watuhumiwa watatu wa ujambazi, walikamatwa eneo la Kiwalani Kwa Mkude jijini Dar es Salaam wakiwa na bastola moja.

Post a Comment

0 Comments