Header Ads Widget

Rais Magufuli atangaza vita na mafisadi, wauza dawa za kulevya 2016





RAIS Dk. John Magufuli, amesema Watanzania wote wanapaswa kuendelea kumuombea ili aendelee na kazi yake ya kupambana na mafisadi wahujumu uchumi na vigogo wauza dawa za kulevya nchini.


Kauli hiyo iliitoa katika mkesha mkubwa wa kuliombea Taifa pamoja na kuuaga mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka 2016, uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.


Rais Magufuli amesema Taifa hili kwa kipindi kirefu lilikabiliwa na vigogo wauza dawa za kulevya, watumishi na vigogo wakwepaji wa kodi pamoja na wizi wa dawa mahospitalini hivyo viongozi wa dini na Watanzania wote wanapaswa kumuombea ili aweze kutumbua majipu ya mafisadi hao.


Amesema ubadhilifu wa mali za umma umekuwa ukichangia kuzorotesha maendeleo ya Watanzania wote kutokana na watu wachache wasiokuwa waadilifu serikalini kuendelea na vitendo vya rushwa huku wengi wakiendelea kutaabika.


Dk. Magufuli ambaye aliwakilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi, William Lukuvi, amesema kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuendelea kuliombea Taifa na kuwaombea watu wabaya wasiopenda maendeleo waweze kubadilika ili nchi iweze kusonga mbele.


“Viongozi wa dini tunapaswa kuendelea kumuombea rais wetu (Dk. John Magufuli) aendelee kutumbua majipu haya ambayo yanasababisha maendeleo ya Taifa letu kurudi nyuma.


“Watanzania wenzangu tunapaswa kuendelea kuwa wamoja na kumuunga mkono Rais Magufuli (John Magufuli) aendelee kufanya kazi yake zaidi, kuna wizi wa dawa katika vituo vya Afya watumishi wazembe ambao hawafanyi kazi ya umma vizuri sasa hayo yote yanahitaji ushirikiano wetu kwa rais aweze kusimamia,” amesema Lukuvi.


Hata hivyo katika salamu zake, aliwataka Watanzania wote kwa ujumla bila kujali itikadi za vyama na dini zao kuendeleza umoja na mshikamano na amani iliyopo tangu Taifa hili linapata uhuru mwaka 1964.


Hata hivyo tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani ameweza kuwang’oa vigogo kadhaa katika nyadhifa zao kwa tuhuma mbalimbali, kitendo ambacho kimeonekana kuwachukiza baadhi ya viongozi na watumishi wa umma ‘mafisadi’.


Baadhi ya viongozi waliong’olewa mpaka sasa ni aliyekuwa Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Rished Bande, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).


Viongozi wengine waliondolewa katika nyadhifa zao ni Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Diwani Msemo, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam (DART), Asheria Mlambo na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali Reli Tanzania (RAHCO), Benhadard Tito.


Pamoja na kuwang’oa vigogo hao, pia baadhi ta watumishi kwenye taasisi hizo nao wameguswa na fagio lililowaondoa katika nafasi zao, kwa sababu ya kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili huku na wengine wakigikishwa mahakamani.


Naye Askofu Geoffrey Manashi, amesema Watanzania wanapaswa kuendelea kuliombea Taifa kuendelea kuwepo amani kwani bila amani hakuna maendeleo katika taifa lolote lile.


Amesema uchaguzi wa mwaka 2015 watu wengi walikuwa na imani kwamba Taifa hili litaingia katika machafuko lakini mwenyezi Mungu aliweza kulivusha salama na kufanikiwa kumpata Rais Dk. John Magufuli, ambaye ameweza kufanya kazi yake kwa kasi kubwa ambayo watu wengi walitarajia.


Naye Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, Nape Nnauye amesema kuwa baadhi ya wanasiasa na wananchi walidhani Taifa litaingia katika vurugu na machafuko lakini wameshangaa kuona uchaguzi umemalizika kwa amani.


“Wapo waliodhani tutaingia kwenye machafuko, lakini imeshindikana, hiyo yote ni kutokana na Mungu wetu kutuvusha salama na tumepata rais mzuri ambaye sasa hivi nchi nyingi zinatamani ziwe nae,” amesema Nnauye.


Naye Askofu kutoka nchini Kongo, Debora Sanganyi, amesema Watanzania wanapaswa kuwaombea wakongo na wao waendelee kuwa na amani iliyopo hapa nchini kwetu.


Amesema kuwa Kongo na wao wanatarajia kufanya uchaguzi mkuu hivyo Watanzania wanapaswa kuwaombea na kumpata rais mchapa kazi kama Rais John Magufuli.


“Jamani na sisi wakongo mtuombeeni kuvuka salama yale yanayokuja, tupate rais mzuri kama wa kwenu, watanzania tuombeeni ndugu zenu,” amesema Sanganyi.
Mpekuzi blog

Post a Comment

0 Comments