(Pichani ni Watoto walioathirika na Polio. Picha kwa hisani ya shirika la WHO).
Na Magreth Kinabo.
TANZANIA imetangazwa rasmi kuwa ni mojawapo ya nchi isiyokuwa na ugonjwa wa polio katika nchi za Afrika katika mkutano wa Tume ya Afrika ya kuthibitishwa kutokomezwa kwa polio(Afrika Regional Certification Commission for Polio Eradication).
Kutangazwa kulifanyika katika mkutano huo uliofanyika nchini Madagascar, Novemba 26, mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Donan Mmbando wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu ugonjwa huo ulifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam.
“Hii inamaanisha kuwa kwa sasa hatuna ugonjwa wa polio tena nchini kwa sababu tumeweza kuwafikia watoto wengi zaidi kwa kuwapatia chanjo ya polio na hivyo kuongeza kinga kwenye jamii.Kutokana na mafanikio hayo, tunatakiwa bado kuendelea na kutoa chanjo ya polio kwa watoto wote stahiki ili kuongeza kinga kwa jamii pamoja kuimarisha mfumo wa ufutiliaji wa mgonjwa yoyote mwenye ulemavu wa ghafla,” alisema Dkt. Mmbando.
Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba mgonjwa wa mwisho wa polio alipatikana Julai mwaka 1996 hapa nchini.
Aliongeza kuwa ufuatiliaji wa magonjwa yanayokingwa na chanjo uliimarishwa na kufikia viwango vinavyo kukubalika kimataifa na kuthibitisha kuwa watoto wenye umri chini ya miaka 15 waliopata ulemavu wa ghafla wanapatikana na sampuli zao kuchukuliwa mara moja.
Hivyo kuanzia mwaka 1997 mpaka Oktoba 2015 jumla ya sampuli 6,249 za watoto waliopata ulemavu zilipelekwa kwenye maabara za kimataifa na kuthibitishwa kuwa hakuna sampuli iliyoonesha uwepo wa ugonjwa wa polio.
Dkt. Mmbando aliongeza kwamba wizara yake kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo imekuwa ikihakikisha kwamba watoto wote Tanzania wanapata chanjo zenye ubora ili kuwakinga dhidi ya magonjwa ya milipuko ikiwemo ugonjwa wa polio.
“ Mwitikio wa wananchi kwa huduma za chanjo umeendelea kuwa mkubwa kwa takribani miaka kumi iliyopita na kufikia viwango vya zaidi ya asilimia 90 kwa kila chanjo kitaifa na wilaya zaidi ya asilimia 80 kufanya vizuri katika kutoa huduma za chanjo,” alisema Dkt. Mmbando.
Ugonjwa wa polio ni ugonjwa wa kuambukizwa unaosababishwa na virusi vya polio, unaathiri misuli na mfumo wa fahamu hivyo kusababisha kupooza kwa viungo hasa na miguu na wakati mwingine kusababisha hata kifo .
Alisema ulemavu huo ukishajitokeza huwa ni wa kudumu, waathirika wakuu wa ugonjwa huo ni watoto hasa waliaochini ya umri wa miaka mitano.
Aliongeza kwamba ugonjwa huo unazuilika kwa chanjo ya polio ambayo ni salama na inatolewa bure na Serikali katika vituo vyote vya huduma ya afya.
Dkt. Mmbando alitoa pongezi kwa wananchi wote wakiwemo viongozi na watendaji wa ngazi zote kwa ushirikiano wao ambao umeifikisha Tanzania kwenye ramani ya dunia ya kutokuwa na ugonjwa huo.
Aidha wizara imewashukuru wajumbe wa kamati mbalimbali za kutokomeza ugonjwa huo chini ya uongozi wa Profesa Ester Mwaikambo, watendaji wa Mpango wa Taifa wa Chanjo na wadau wa chanjo, wadau wa mfuko wa pamoja wa Pamoja wa Afya , WHO, GAVI, UNICEF, CHAI, USAID,
REDCROSS NA LIONS CLUB kwa kazi kubwa ya kuhakikisha kila mtoto mlengwa anapata chanjo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi nne ambazo zimepata cheti hicho mwaka huu, katika bara hilo.Pia ni nchi ya 33 kati ya nchi 47 za bara hilo ziliowahi kupata cheti hicho.
Katika bara hilo bado nchi 14 ambazo hazijawahi kupata cheti hicho.
0 Comments