Header Ads Widget

Operesheni Kuondoa Wafugaji yasitishwa......Askari wa Wanyamapori Wanaonyanyasa Wafugaji Wapewa Onyo





MAWAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na wa Maliasili na Utalii, wameonya askari wa Wanyamapori wanaojihusisha na utesaji, unyanyasaji na kujipatia fedha haramu kwa kukamata mifugo au wakulima, waache mara moja badala yake, wazingatie maadili ya kazi yao.

Aidha, Serikali imetangaza kusitishwa kwa operesheni za kuwaondoa wafugaji kwenye maeneo wanayochungia mifugo ikiwemo mapori tengefu, wakati ukifanyika utaratibu wa kuwawezesha kuendesha shughuli zao.

Matamko hayo yalitolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani, kupitia mkutano uliofanyika kati ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba na wafugaji, wakulima wa Kanda ya Ziwa.

Tamko la mawaziri hao ambalo ni sehemu ya mikakati yao ya kukomesha kero kwa wakulima na wafugaji, limekuja huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, kuhakikisha wanaongeza udhibiti na usimamizi wa migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao husika.

Katika mkutano uliofanyika juzi katika uwanja wa Mnadani (Benaco) Ngara, mkoani Kagera, Mwigulu aliongozana na Makani ikiwa ni sehemu ya kusikiliza kero na kutafuta utatuzi wa kudumu wa tatizo la malisho linalowakabili wafugaji.

Wafugaji kupitia Chama cha Wafugaji wa Kanda ya Ziwa (Chawakazi) walilalamikia uonevu kutoka kwa baadhi ya askari wa Wanyamapori na wakaomba serikali iachane na operesheni ya kuwaondoa wafugaji kutoka kwenye maeneo yanayotumika kuchunga ng’ombe katika pori la Burigi.

Baada ya kusikiliza malalamiko ya makundi hayo, pia Mwigulu alimuomba Naibu Waziri Maliasili kupitia ofisi yake, kuangalia uwezekano wa kupitia upya mapori tengevu ili baadhi wapewe wafugaji na wakulima kwa shughuli zao.

Akitangaza kusitishwa kwa operesheni za kuwaondoa wafugaji kwenye mapori, Makani aliahidi ofisi yake itafanya haraka iwezekanavyo utaratibu unaoendelea wa kupitia mapori 17 ukamilike ili kutoa maeneo kwa watu wafanye shughuli zao za kilimo na ufugaji.

Akisisitiza askari Wanyamapori kuzingatia maadili ya kazi yao, Makani alisisitiza kwamba Serikali itachukua hatua kuhakikisha askari wote wanafanya kazi kwa kuheshimu sheria za nchi.

Akizungumza na viongozi wa mkoa wa Lindi hivi karibuni, Waziri Mkuu, Kassim, aliagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, kudhibiti migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao.

Waziri Mkuu alisema, “Ardhi ni mali ya Serikali lakini maeneo yanayotwaliwa kwa sababu mbalimbali za maendeleo yasiwe chanzo cha migogoro na wananchi tunaowaongoza.”


Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema anatambua kuna mgogoro wa eneo la mgodi katika wilaya ya Ruangwa baina ya wananchi na wawekezaji wa kampuni ya Uranex.

Na hii ni kwa sababu wao ndiyo waliamua kufanya tathmini ya eneo hilo. “Yale ni makosa kwa sababu aliyepaswa kufanya tathmini ni Halmashauri na siyo mwekezaji,” alisema.
CHANZO: Mpekuzi blog

Post a Comment

0 Comments