Urafiki wa Jaji Joseph wariona na chama chake cha CCM uliofufuka wakati wa Uchaguzi Mkuu, unaweza kuingia tena doa baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kusema iwapo Serikali itaanza harakati za kumalizia mchakato wa Katiba, atatoa yake ya moyoni.
Jaji Warioba, aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alishambuliwa na makada wa chama hicho kutokana na kuwasilisha Rasimu ya Katiba iliyotofautiana na utashi wa CCM, hasa kwenye suala la muundo wa Muungano kuwa wa serikali tatu.
Lakini tofauti hizo zilipotea wakati wa Uchaguzi Mkuu alipoamua kusimama kidete kumtetea mgombea urais wa CCM bila ya kujali kilichomsibu kwenye Bunge la Katiba.
Baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe kueleza kuwa Rais John Magufuli amemuagiza aendelee na mchakato wa Katiba kuanzia pale alipoishia, Jaji Warioba amehifadhi maoni yake, lakini anasema ana yake ya moyoni.
“Kwa sasa siwezi kusema chochote kuhusu kauli ya Serikali kuendelea na mchakato wa Katiba,” alisema Jaji Warioba alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kauli hiyo ya Dk Mwakyembe.
“Nasubiri nione. Pale watakapoanzia tu, ndiyo nitasema.”
Jaji Warioba alikuwa mmoja wa wadau mbalimbali walihojiwa na gazeti hili kuhusu mwenendo wa suala hilo lililogharimu mamilioni ya fedha za walipa kodi.
Wadau wengi walishauri mchakato huo kuanzia kwenye Rasimu ya Katiba na kutafutwa maridhiano kabla ya kuendelea na suala hilo la kuandika Katiba Mpya kuibadili ya sasa iliyoandikwa mwaka 1977.
Mchakato wa Katiba ulisitishwa mapema Aprili wakati ukisubiri hatua ya mwisho ya kupiga Kura ya Maoni kutokana na kutokamilika kwa uandikishaji wapigakura. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilisema imeamua kuahirisha Kura ya Maoni iliyokuwa ipigwe Aprili 30 kwa kuwa kazi hiyo ya kuandikisha wapigakura ilikuwa haijakamilika na haikusema mchakato huo utaendelea lini.
Lakini hivi karibuni, Dk Mwakyembe alisema Rais amempa kazi ya kumalizia mchakato wa Katiba kutoka pale ulipoishia, akimaanisha upigaji wa Kura ya Maoni, jambo ambalo limepingwa vikali na wadau hao.
Mmoja wa wadau hao, Deus Kibamba, ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), alisema iwapo mchakato huo utaendelea bila ya kutafuta maridhiano, hakutakuwa na Katiba Mpya.
“Mchakato wa Katiba Mpya ni jipu linalosubiri kutumbuka,” alisema Kibamba.
“Wakiendelea na mchakato huo bila kwanza kufanyika kwa maridhiano, watapata kashfa kubwa maana tutapata Katiba ambayo si mpya.”
Alisema busara inayotakiwa kufanyika sasa ni kuitishwa kwa jopo la watalaamu watakaoichambua Rasimu ya Katiba na Katiba Inayopendekezwa na kutoa ushauri wa kuendelea na mchakato huo.
“Tumetoa ushauri wa mambo mengi, lakini yalipuuzwa. Hili si jambo la kulazimisha. Huwezi kuendelea wakati kuna pande mbili zinapingana, hii ni hatari kwa kitu muhimu kama hiki ambacho ndicho kitakachotupa dira na mwelekeo wa taifa letu,” alisema.
Alisema kilichozungumzwa na Dk Mwakyembe ni mwendelezo wa “kutoambilika” kwa wale waliotakiwa kuutazama upya mchakato wa kupata Katiba Mpya baada ya kuonekana kuwa na kasoro nyingi.
Alikuwa akizungumzia kugawanyika kwa Bunge la Katiba baada ya wajumbe kutoka vyama vinne vya NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF kususia vikao kwa madai kuwa Bunge liliacha kujadili maoni ya wananchi na kuingiza utashi wa chama tawala cha CCM. Vyama hivyo viliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushirikiana kulisukuma Bunge lirudie Rasimu ya Katiba.
Profesa Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha St Augustine, pia alizungumzia mgawanyiko uliojitokeza kwenye Bunge la Katiba akitaka kuwapo na maridhiano kwanza.
“Bunge la Katiba lilikwenda mrama na liliwagawa wananchi. Wajumbe wa Bunge hilo walipitisha mambo ambayo hayakutolewa maoni na wananchi. Walifumba macho wakadhani Katiba itapatikana lakini imeshindikana,” alisema Profesa Baregu.
“Rais Magufuli anapaswa kuwa na hekima na atambue wazi kuwa Katiba Inayopendekezwa si sahihi. Katiba sahihi ni ile iliyotolewa na Tume ya Warioba ambayo iliweka mabadiliko ya kiutawala, uongozi na maadili,” alisema.
Alisema kuwa mchakato huo unapaswa kuanzia pale ambako baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba waliposusia vikao vya Bunge hilo, kutokana na kuanza kuchakachuliwa kwa maoni ya wananchi yaliyokuwamo katika Rasimu ya Katiba.
Profesa Baregu alitaja mambo mawili yanayoweza kufanyika kuwa ni kutafuta watalaamu wa sheria na katiba ili kuwatumia kuandaa Katiba Mpya.
“Hawa watazungumza na wadau mbalimbali na kuja na Katiba hiyo. Jambo hili walilifanya wenzetu wa Kenya na walifanikiwa,” alisema.
“Pili, liundwe upya Bunge la Katiba na kuichambua Rasimu ya Katiba chini ya msaada na ushauri wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo iliyopita kwa wananchi na kukusanya maoni. Tutazame masilahi ya Taifa letu. Tutazame pale tulipojikwaa.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally pia alizungumzia kugawanyika kwa Bunge la Katiba.
“Mchakato mzima ulikumbwa na sintofahamu kubwa na kuligawa Taifa, sasa wanaposema wanaendelea walipoishia kivipi?” alihoji.
Alisema wengi wanadhani kinachopaswa kufanyika sasa ni Watanzania kupiga Kura ya Maoni, jambo ambalo alidai haliwezekani kufanyika bila kupatikana kwa muafaka wa pande mbili zinazovutana.
“Lazima umalize mvutano kwanza maana kasoro zilikuwa nyingi. Kila ngazi ya mchakato huo haikuwa na muafaka, kuanzia uundwaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sasa hivi utaona (mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Katiba, Jaji Joseph) Warioba anasimama kwenye majukwaa ya CCM na kukiunga mkono chama chake.
“Pia aliyekuwa mjumbe wa tume hiyo, Profesa Mwesiga naye anasimama kwenye majukwaa ya Chadema na kukiunga mkono chama hicho,” alisema Bashiru, ambaye aliufananisha mchakato huo na kiporo chenye sumu.
“Kama wanataka kumaliza tatizo ni lazima watazame tangu mchakato huu ulipoanza na kujua tatizo lilikuwa nini na si kuendelea tu hivihivi.”
Profesa wa Chuo Kikuu Ruaha, Gaudence Mpangala alisema kupiga kura kupitisha Katiba Inayopendekezwa haitawezekana na badala yake akashauri kuundwa kwa Bunge jipya la katiba.
“Tuliona wajumbe 201 walioteuliwa na Rais walivyokuwa makada wa vyama vya siasa. Bunge la Katiba ni suala la kitaifa si vyama,” alisema.
Profesa huyo alisisitiza kwa hali ilivyo sasa, gharama haziepukiki ni lazima Bunge la Katiba liundwe upya kwa ajili ya kuichambua upya Rasimu ya Katiba ambayo ilitokana na maoni ya wananchi yaliyoondolewa katika Katiba Inayopendekezwa.
Kauli ya Sitta
Hata hivyo, Samuel Sitta, aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba, alipingana na maoni ya kuanza upya mchakato akisema tayari fedha nyingi zimetumika na kinachotakiwa kufanyika sasa ni mchakato kuendelea pale ulipoishia.
Kuhusu mvutano ulioibuka katika Bunge la Katiba, Sitta alisema: “Bunge lile lilikuwa na wajumbe 654. Ni wajumbe 114 tu ndiyo walitoka kwa kudai kwamba rasimu ya pili ya Warioba haifuatwi.
“Kusema kwamba hawa 114 ndiyo wanajua wananchi wanataka nini kuliko hawa 543 ni msimamo usio sahihi. Kwa nini watu 543 waonekane wote ni wajinga.”
Alisema hata wanaolalamikia kuwa suala la maadili limeondolewa katika Katiba Inayopendekezwa hawako sahihi, kwa maelezo kuwa katika Raismu ya Katiba jambo hilo liliwekwa katika Tunu za Taifa, katika Katiba Inayopendekezwa, maadili limewekwa katika utawala bora.
Alipoulizwa kuhusu mkanganyiko wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kuruhusu kuendelea kwa mchakato huo alisema: “Hayo ni juu ya Serikali. Watakwenda bungeni na watajua cha kufanya. Serikali ichague njia ambayo haiingizi gharama ya mabilioni kwa nchi.”
CHANZAO:UDAKUSPECIALLY
0 Comments