Header Ads Widget

Wanafunzi wakithiri kutazama picha za ngono katika simu zao



BARAZA la Ushauri la Watumiaji Huduma za Mawasiliano Mkoa wa Iringa (TCRA-CCC) limewahadharisha vijana na matumizi yasiofaa ya huduma mbalimbali zinazotolewa kupitia simu za mkononi.

“Picha za ngono na utafutaji wa wapenzi wapya ni sehemu ya huduma katika simu za mkononi zinazowavutia vijana wengi wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo,” alisema Mwenyekiti wa baraza hilo, Raphael Mtitu.

Mtitu alisema kwa kupitia huduma za Whatsapp na Facebook, wanafunzi wamekuwa wakikutana na marafiki wapya wanaowataka kimapenzi lakini pia wamekuwa wakibadilishana picha mbalimbali za ngono zinazokinzana na maadili ya Mtanzania.

“Kuna picha za video za ajabu zinatumwa kupitia mitandao hiyo. Picha hizo ambazo kiukweli hazifai kutazamwa na vijana wetu zimekuwa kivutio chao kikubwa,” alisema.

Alisema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapaswa kulitazama hilo na kulifanyia kazi ili kunusuru kundi kubwa la vijana linalobomoka kimaadili kutokana na matumizi ya huduma hizo katika simu za mkononi.

Naye Katibu wa Baraza, Edina Byemerwa alisema baadhi ya sinema zinazoigizwa na Watanzania nazo zinachangia kumomonyoa maadili ya Mtanzania.

“Ni sinema zinazooneshwa bila kipingamizi chochote, na ndizo zinazoelekea kupendwa zaidi na vijana wetu tu kwa sababu zinazungumza mapenzi zaidi.

“Nyingi ni za mapenzi, zinahusu vijana wa kike na kiume kutafutana kimapenzi; hatujui vijana wetu wanazipendea nini lakini kwa vyovyote yapo wanayojifunza na hayo yanaweza kuwa ya hatari katika maisha yao,” alisema.

Byemerwa alisema TCRA haijatimiza wajibu wake katika kusimamia Sekta ya Utangazaji na ndio sababu yapo mengi yanafanyika kinyume na sheria.

Bila kutoa mifano ya filamu hizo, Byemerwa alisema kama TCRA itaendelea kuzifumbia macho zitaendelea kuharibu rika la vijana wengi.

Post a Comment

0 Comments