Header Ads Widget

SASA DAR ES SALAAM KUFUNGWA KAMERA ZA MATUKIO





NASRA ABDALLAH, Dar Es Salaam, Tanzania
RAIS Jakaya Kikwete, amesema kuanzia Juni mwakani kila kinachofanyika katika jiji la Dar es Salaam kinaonekana katika mitambo itakayokuwapo kila mahali.


Alisema kutokana na kufungwa kwa mitambo hiyo waharibifu wa miundombinu, vibaka na wahalifu hawatoweza kufisha matendo yao.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kufungua barabara ya Tegeta – Mwenge iliyojengwa kwa kiwango cha lami huku ikiwa na urefu wa kilometa 12.9.


Alisema inasikitisha kuona serikali ikiingia gharama kubwa katika kutengeneza barabara halafu watu wasiokuwa na uchungu na fedha hizo za walipa kodi wakiharibu miundombinu hiyo kwa maslahi ya matumbo yao.




“Tumeshaongea vya kutosha jamani katika hili sasa dawa ya watu wa aina hii ipo jikoni na Juni mwakani watu wote hawa tutawakamata kirahisi tu hawatakuwa na pa kukimbilia,”alisema.


Hata hivyo Rais Kikwete, hakuwa tayari kueleza ni mitambo ya aina gani itakayofungwa lakini katika nchi mbalimbali kumekuwa na kamera katika mitaa ambazo zinarekodi kila kinachofanyika.


Aliongeza kuwa ujenzi wa barabara ya Tegeta-Mwenge, itasaidia kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam na hii ni baada ya kukaribia kumalizika kwa barabara ya Msata Bagamoyo.


Alisema kutokana na tatizo la foleni lililopo katika Jiji hilo, ambapo hata mihadi ya watu kukutana siku hizi imekuwa ni taabu, Serikali imekuwa ikijitahidi kutafuta njia mbalimbali za kutatua kero hiyo ikiwemo kuboresha vyombo vya usafiri wa umma na utengenezaji wa barabara za mchepuko.


Hata hivyo aliwataka wananchi kujua kuwa tatizo la foleni halipo tu Dar es Salaam bali hata kwanye nchi zilizoendelea ikiwemo Newyork Marekani na China.


Rais Kikwete, alisema hii inachangiwa na kukua kwa maendeleo ambapo kwa Tanzania mwaka 1980 magari yaliyokuwa yakipita barabarani ni yale ya Serikali na kwa watu binafsi ilikuwa lazima uombe kibali kabla ya kununua gari.


“Lakini hivi sasa familia nyingi zinamiliki magari na nyingine zimeenda mbali zaidi ambapo baba ana gari lake, mama na watoto na bado watu wataendelea kumiliki magari siku za baadaye yote hii imechangiwa na kubadilika kwa mfumo wa maisha na nchi kupiga hatua ya maendeleo kwa watu wake,”alisema.


Alisema ameziagiza Mamlaka husika kuboresha usafiri wa reli kwa kuongeza njia za reli katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuleta mabehewa yatakayoendana mahitaji.


Alisema pia serikali ipo mbioni kuanzisha kivuko kitakachotoa huduma kwa wakazi wa Bagamoyo na Tegeta na kujenga miji mingine nje ya mji ili huduma zinazofuatwa mjini zipatikane huko huko walipo.


Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Alhaj Mussa Iyombe, alisema barabara hiyo imetengenezwa kwa msaada mkubwa wa Serikali ya Japan ambako shilingi bilioni 99.6 zimetumika kukamilisha mradi huo.


Naye Balozi wa Japan hapa nchini, Masaki Okada, alisema Serikali yake inaamini kuwa barabara ni kichocheo kikubwa katika ukuaji wa uchumi na kipaumbele chake cha kwanza ni ujenzi wa barabara.

Post a Comment

0 Comments