Header Ads Widget

VURUGU ZAIBUKA KILOSA MOROGORO, POLISI WALAZIMIKA KUTUMIA MABOMU


Vurugu kubwa zimezuka katika tarafa ya Magole wilayani Kilosa jana ambapo polisi ililazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto ili kuwatawanya wananchi. 
Vurugu hizo zilisababishwa na wananchi wa vijiji vitatu vya Mabana, Mateteni na Mbigili baada ya kuvamia eneo la Mahakama ya Magole na kutaka kuichoma moto wakishinikiza kuachiwa kwa wenzao waliokuwa wamekamatwa. 
Vurugu hizo zilitokea majira ya saa 5 asubuhi wakati wananchi hao walipokusanyika na kufanya maandamano hadi katika mahakama hiyo wakitaka wakulima wenzao 12 waliokamatwa kwa madai ya kuvamia na kulima shamba lililotengwa na serikali. 
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Rajabu, alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni askari polisi katika mji wa Dumila kwenda kuwakamata wakulima hao katika shamba hilo eneo la Mkongeni ambalo zamani lilikuwa likilimwa na waliokuwa wapigania uhuru wa Afrika Kusini. 
Alisema kuwa katika siku za hivi karibuni wakulima wa vijiji hivyo waliamua kuvamia na kuanza kulima bila kufanya mawasiliano na serikali wakati eneo hilo tayari lilikuwa limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo kikuu cha Sayansi. 
Alisema kuwa polisi ilifika katika eneo la shamba hilo na kukuta makundi hayo ya wakulima na ndipo likafanikiwa kuwakamata baadhi yao na kuwapeleka mahakamani kwa ajili ya kuwasomea mashtaka baada ya wengine kukimbia. 
Ilidaiwa kuwa waliokimbia walienda kujikusanya katika vijiji hivyo vitatu na kufanya maandamano hadi katika mahakama hiyo na kuanza kufanya vurugu za kutaka kuchoma moto na kurushia mawe baadhi ya askari wakishinikiza kuachiwa wenzao. 
Mtoa habari huyo alidai kuwa polisi walizidiwa nguvu na kulazimika kuomba msaada wa askari wengine kutoka wilaya ya Mvomero ambao walifika na kuanza kutawanya wananchi hao kwa kuwarushia mabomu ya machozi pamoja na kupiga risasi za moto hewani.

Post a Comment

0 Comments