MONROVIA, LIBERIA WANAUME waliokuwa na silaha waliodai kwamba hakuna maradhi ya Ebola Liberia, walivamia eneo ambalo wanaougua ugonjwa huo walikuwa wametengwa jijini Monrovia.
Walioshuhudia kisa hicho kilichotokea Jumapili walisema wakati wa uvamizi huo, wagonjwa 20 walioambukizwa virusi vya ugonjwa huo walitoroka. “Walivunja mlango na kupora mali eneo hilo.
Wagonjwa wote wametoroka,” alisema Bi Rebecca Wesseh, aliyeshuhudia uvamizi huo. Mkuu wa chama cha wahudumu wa afya wa Liberia, Bw George Williams na wakazi wa jiji hilo walithibitisha ripoti hizo.
Williams alisema eneo hilo lilikuwa na wagonjwa 29 waliokuwa wakichunguzwa kabla ya kupelekwa hospitali. Hata hivyo, haikubainika idadi ya wagonjwa ambao hawakujulikani waliko.
“Wote walipatikana kuwa na Ebola,” alisema na kuongeza bila kufafanua kuwa tisa walikufa. Bi Wesseh alisema alisikia wavamizi hao wakipiga kelele wakisema Rais Ellen Johnson Sirleaf “ hana pesa,” na kuongeza “ anatafuta pesa. Hakuna Ebola Liberia.”
Wesseh alisema wavamizi hao ambao wengi waliokuwa vijana waliobeba rungu walivunja mlango wa eneo lililotengwa kwa wagonjwa katika shule moja ya pili viungani mwa Monrovia.
0 Comments