Header Ads Widget

MFANYABIASHARA WA MADINI AJIUA KWA KUJIPIGA RISASI AKIKWEPA KUFIA MIKONONI MWA WANANCHI WENYE HASIRA KALI


MFANYABIASHARA maarufu wa madini ya dhahabu amejiua kwa kujipiga risasi kichwani. Amefanya hivyo wakati akiwakimbia wananchi wenye hasira na wachimbaji wadogo kwenye machimbo ya Kalole Kata ya Bugarama wilaya ya Kahama, baada ya kumjeruhi mguuni kwa kumpiga risasi mchimbaji mdogo wa machimbo hayo.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alisema ofisini kwake mjini hapa jana kuwa tukio hilo ni la juzi saa 12 jioni kwenye machimbo hayo.

Alimtaja mfanyabiashara huyo ni Mwigulu David (34) na kwamba inadaiwa alikuwa akiwadai wafanyabiashara wenzake mgawo wake wa dhahabu, waliyowapunja wachimbaji.

''Katika purukushani hiyo, Mwigulu alikuwa akimhoji mmoja wa wafanyabiashara wenzake katika mzozo wa kugawana dhahabu waliyowapunja wachimbaji,” alisema Kamanda.

Kamanda alisema, “Mwigulu alichomoa bastola yake kutoka mfukoni kwa lengo la kutaka kumshambulia mmoja wa wafanyabiashara wenzake na kwa bahati mbaya risasi ikamjeruhi kwenye mguu wa kushoto mchimbaji Maduhu Amos (25) na kusababisha akimbizwe hospitali kwa matibabu.''

Kutokana na kitendo hicho, wananchi wakiwemo wachimbaji wadogo walimzonga mfanyabiashara huyo.

Inadaiwa alipoona hali imebadilika huku watu wengi wakitaka kumpiga, aliingia kwenye gari lake na kuliondoa kwa kasi, akitaka kujinusuru kwa kipigo cha wananchi wenye hasira.

Akiwa njiani alikuta barabara kuu, inayotoka kwenye machimbo hayo kwenda mjini Kahama ikiwa imezibwa kwa kuwekewa magogo na mawe makubwa huku gari likishambuliwa kwa mawe kutoka pande zote.

“Aliamua kuteremka kwenye gari na kukimbilia kwenye moja ya nyumba zilizopo kando ya barabara hiyo na kujifungia, lakini hata hivyo wananchi waliokuwa wakikimbiza gari hilo waliendelea kurusha mawe na kutishia kuvunja milango na kuichoma moto nyumba hiyo,” alisema kamanda.

Kulingana na maelezo ya kamanda, Mwigulu akiwa amejifungia aliamua kujipiga risasi tatu kichwani zilizosababisha kifo chake papo hapo.

Post a Comment

0 Comments