Header Ads Widget

HATIMAYE POLISI ALIYEFUKUZWA KAZI AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUJIANDAA KUFANYA UHALIFU





Askari Polisi aliyefukuzwa kazi kwa utovu wa nidhamu mwaka 2012 baada ya kukutwa na silaha katika ukumbi wa disko mkoani Kilimanjaro, James Marwa (26) amekamatwa na Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime-Rorya akidaiwa kuwa katika harakati za kwenda kufanya uhalifu eneo la mgodi wa Nyamongo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime-Rorya, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kukamatwa kwa Marwa.

Mambosasa alisema kwa sasa anashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya riffle ikiwa na risasi tano ya kampuni ya ulinzi ya Paroma Security na kukiri kwamba alikuwa anaenda kuungana na wenzake kwenda kufanya uhalifu mgodi wa Nyamongo.

Akifafanua Kamanda Mambosasa alisema Julai 29 walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuonekana mtuhumiwa maeneo ya Mtaa wa Magamaga, kata ya Sabasaba, Tarime, akiwa na bunduki aina ya riffle yenye namba 58368 TZCAR 5963 ikiwa na risasi tano.

“Tulifuatilia na kumkamata mtuhumiwa akiwa na silaha hiyo, tumemhoji na kubaini kuwa kwa hivi sasa alikuwa akifanya kazi ya ulinzi katika kampuni ya ulinzi ya Paroma Security eneo la ujenzi wa Mizani huko Sirari na alipohojiwa zaidi alidai alikuwa akienda Nyamongo mgodini kuungana na wenzake kufanya Uhalifu,” alisema Kamanda.

Alisema watamfikisha mtuhumiwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

Post a Comment

0 Comments