Kamati ya Mashauriano ya Bunge Maalumu la Katiba imetoa mapendekezo kwa Kamati ya Uongozi kwamba Bunge Maalumu liendelee na mkutano wake wa pili wa Bunge hilo kuanzia Agosti 5 mwaka huu.
Katika ngwe hiyo ya pili mkutano huo uzingatie upya baadhi ya kanuni za Bunge hilo ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kazi ya kujadili na kupitisha katiba inayopendekezwa inakamilika kwa siku 63 zilizosalia kisheria.
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta alisema kamati hiyo imetoa sababu za kuendelea na ngwe ya pili ya bunge hilo inatokana na kuwepo masuala mengi muhimu ya kikatiba ambayo yanawaunganisha.
Alitaja mambo hayo kuwa ni kama usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi, kuikarabati Tume ya Uchaguzi, kurekebisha kikatiba masuala ya Muungano, haki za wakulima, wafugaji, wasanii, ukomo wa vipindi vya uongozi na mengineyo.
Akitoa maoni na ushauri wa kamati hiyo kwa wananchi katika taarifa yake iliyosomwa jana na Katibu wake, Yahya Khamis Hamad alisema ngwe ya pili imebakiwa na siku 60 kisheria na nyongeza tatu zilizokuwa pungufu kufika 70 za awali na kueleza kuwa wajumbe wa kamati hiyo wameshangazwa na wenzao kugomea hata kikao cha mashauriano.
Alisema kuanzia sasa bunge litaanza kujibu upotoshwaji kuhusu mchakato wa Katiba kadri utakavyojitokeza kutokana na baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kwenda kwa wananchi na kuwapotosha wananchi.
Sitta alisema kamati imegundua mapungufu yaliyochangia kukuza tatizo lililopo la baadhi ya wajumbe kugomea vikao kuwa ni pamoja na wajumbe wanaosusia mchakato huo kutambuliwa kama kundi rasmi la bunge hilo wakati makundi rasmi ni wabunge, wawakilishi na lile la wajumbe 201.
“Lazima ielewekwe kuwa wakati wa kura za maamuzi makundi rasmi ni kundi la wajumbe kutoka Tanzania bara na wa Tanzania Zanzibar na siyo kundi hilo, ”alisema.
Sitta alisema sababu nyingine ni Sheria ya mabadiliko ya Katiba hata kanuni za bunge kutokuwa na vipengele vinavyozuia utoro, ukosefu wa nidhamu na matendo mengine yanayolenga kuvuruga mchakato huo.
Alisema kamati inaona kwamba kitendo cha kuendelea kususia bunge na kupuuza mwito wa jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini inatia shaka dhamira halisi ya viongozi wa kundi hilo la wasusiaji.
“Kupuuzia juhudi zote za usuluhishi kunazua mashaka kuhusu lengo la wasusiaji kwamba pengine agenda ya viongozi hao ni nyingine na sio upatikanaji wa Katiba,” alisema Sitta.
Alisema pia kamati inahoji utamaduni mpya unaoanza kujengeka wa kuendesha mambo kwa kususa, kwani ni vigumu muafaka wa jambo lolote ukapatikana kwa kususia majadiliano na kuendesha kampeni ya maneno nje ya vikao rasmi.
Mwenyekiti huyo alisema kamati inarejea kuwa wajumbe 629 wamekabidhiwa jukumu adhimu na la kihistoria kwa niaba ya Watanzania ambalo hutokea baada ya miongo kadhaa ya uhai wa taifa lolote haitakuwa haki kwa Watanzania ikiwa hakutakuwa na maridhiano yatakayowezesha kukamilisha kazi waliyopewa.
“Pamoja na yote, kamati ya mashauriano inaendelea kutoa mwito kwa wajumbe waliosusa mikutano ya bunge hili kurejea kwani ndilo lenye uwezo wa kutatua matatizo yaliyopo,” alisisitiza.
Sitta alisema mapema mwezi huu wajumbe 30 wa kamati ya mashuriano waliteuliwa lakini kikao kilichofanyika juzi wajumbe wa vyama vya CUF, Chadema na NCCR- Mageuzi walisusia kikao licha ya jitihada za Mwenyekiti na Sekretarieti kuwashawishi kwa siku nzima.
Alisema wajumbe waliohudhuria kikao cha kamati hiyo walikuwa zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wote waliendelea na kikao na kufikia maazimio hayo.
Wakati Bunge Maalumu la Katiba kilitarajiwa kuendelea wiki ijayo, Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) limependekeza kuahirishwa kwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya hadi baada ya uchaguzi mkuu kumalizika mwakani, kutokana na wanasiasa kupandwa na joto la uchaguzi.
Hatua hiyo inatokana na sababu zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Hebron Mwakagenda ambaye alisema, inatokana na michakato mikubwa sita ya kitaifa katika kipindi kifupi cha miezi 15.
Mwakagenda alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, kutokana na kuwepo kwa michakato hiyo, wanapendekeza pia kuahirishwa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa ili ufanyike pamoja na uchaguzi mkuu mwakani na kusimamiwa na tume huru ya uchaguzi kwa kutumia daftari la kudumu la mpiga kura litakaloandaliwa mwaka huu.
Alisema pia wanapendekeza kuahirishwa kwa mchakato wa kuandika Katiba mpya hadi baada ya uchaguzi mkuu, ambapo alisema lengo ni kufupisha mkutano ujao wa Bunge Maalumu la Katiba utakaoanza Agosti 5 kutoka siku 60 walizowekewa hadi wiki mbili ili kufanya kazi ya kujadili, kuridhia na kupendekeza ratiba mpya ya mchakato huo.
Akifafanua juu ya kuahirishwa kwa mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba alisema, kwa sasa wanasiasa waliomo ndani ya bunge hilo wamepandwa na joto la uchaguzi na wengi wao wanaangalia zaidi mwakani hivyo ni ngumu kupata katiba ya muda mrefu.
Alisema hata chanzo cha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya bunge sio matusi pekee, bali ni joto la uchaguzi limewapanda jambo linalofanywa na makundi yote ya vyama yaliyomo ndani ya katiba hiyo.
Alifafanua kuwa jukwaa hilo limebaini hata ufa uliopo wa mchakati kati ya wanaopendekeza serikali mbili na tatu ni sehemu ya mivutano ya kisiasa inayotokana na wanasiasa wanaoendelea kujipima umarufu wao wa kisiasa kwa kutumia katiba mpya.
“Kosa lilifanyika tangu mwanzo katika sheria ya mabadiliko ya katiba kwa kuwaingiza wanasiasa wote ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, wanasiasa wamepandwa na joto la uchaguzi na ndio sababu ya malumbano kuibuka kule bungeni.
“Hao Ukawa au Ukiwa kama watu wanavyowaita na Tanzania Kwanza ambalo ni kundi la CCM wasingeweza kugombana kama ingekuwa ni 2006, kwa hiyo ni heri tukaachana na mchakato wa Katiba Mpya kwa sasa,” alisema Kibamba.
0 Comments