Header Ads Widget

MAMA MZAZI AHUKUMIA KWENDA JELA MIAKA 10 BAADA YA KUMUUA MWANAYE WA KUMZAA


MWANAMKE mwenye umri wa miaka 27 (pichani juu), atakaa jela miaka 10 kwa kumuua binti yake aliyekuwa na umri wa miaka 4.


Hata hivyo, Mahakama Kuu jijini Nairobi ilimwachilia mumewe waliyeshtakiwa pamoja kwa kumuua msichana huyo.



Jaji Nicholas Ombija, alimpata Jane Gathigia Maina na hatia ya kutenda kosa hilo, lakini akasema hakumpata mumewe, Walter Njuguna Njoroge, na hatia ya kumuua mtoto wao Anastasia Njoroge, mnamo Oktoba 3 2010 katika kituo cha kibiashara cha Wangige, viungani mwa jiji la Nairobi.



Hukumu ilipokuwa ikitolewa, wawili hao walisimama kizimbani kama maharusi waliosubiri kula viapo vya ndoa, lakini yakawa mazingira tofauti uamuzi wa jaji ulipowatenganisha kwa miaka kumi.



Jaji Ombija alisema ushahidi ulithibitisha kwamba mwanamke huyo alimuua mtoto huyo kwa kumkaba koo na kisha akatupa mwili wake kwenye kisima.



Alisema kwamba hakuna njia yoyote mtoto huyo hangeenda katika kisima hicho na kutumbukia usiku wa manane ilivyodaiwa, ila alitupwa na mama yake aliyetoka kwenda dukani naye usiku huo.

“Baada ya kuchanganua ushahidi uliotolewa, ninampata mshtakiwa wa kwanza na hatia ya kumuua binti yake. Kwa kuzingatia malilio yake na kwamba ni mama mchanga aliye na mtoto aliyezaa akiwa rumande, nitamhukumu kufungwa jela miaka 10,” akasema Jaji Ombija.



Akimwachilia Bw Njoroge, jaji huyo alisema ingawa ni kweli familia hiyo ilikuwa na mzozo wa kifedha kwa sababu ya mtoto huyo aliyezaliwa nje ya ndoa, hakupata ushahidi wa kumhusisha na mauaji hayo.



Kulingana na maelezo ya kesi hiyo, Bw Njoroge alifika nyumbani saa mbili usiku ambao msichana huyo aliuawa, na mkewe akamwambia hakukuwa na unga wa kupika ugali.



Njoroge alimpatia mkewe Sh100 aende dukani kununua unga na akatoka akiandamana na binti yake na huo ulikuwa mwisho wa mtoto huyo kuonekana akiwa hai.



Mkewe aliporejea baada ya nusu saa, alimpata Njoroge kitandani na akamuuliza ikiwa Anastasia alikuwa amerejea nyumbani.



Njoroge alishangaa na akaanza kumtafuta mtoto huyo kwa majirani lakini hakumpata.



Ujumbe

Siku iliyofuata, walipata ujumbe kwenye mlango wa nyumba yao ukiwafahamisha wamtafute mtoto huyo karibu na kisima ambapo mwili wake ulipatikana.



Jaji Ombija alisema kwamba ushahidi ulionyesha kwamba alitaka kumuua mtoto huyo kwa sababu alimzaa nje ya ndoa.



“Kwenda kununua unga kilikuwa kizingizio cha kupata nafasi ya kumuua mtoto huyo. Hakueleza kwa nini alikaa dukani kwa zaidi ya dakika ishirini ilhali duka lilikuwa karibu na nyumba yao,” akasema Jaji Ombija.



Aliongeza kwamba ujumbe uliopatikana asubuhi uliandikwa na mwanamke huyo ili kusaidia mwili wa mtoto kupatikana.



“Ni yeye pekee aliyejua mtoto alikuwa amepotea. Mtaalamu wa maandishi aligundua aliandika ujumbe huo kuthibitisha alijua kilichotendeka kwa mtoto huyo,” akasema.



Baada ya kuachiliwa, Njoroge alisema alimsamehe mkewe kwa kumuua mtoto huyo na hataoa tena bali atamkubali akitoka jela.

Post a Comment

0 Comments