Header Ads Widget

Kikwete awataja Mayele na Saido kuwaamsha wazawa

Kikwete awataja Mayele na Saido kuwaamsha wazawa

Dodoma. Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ameonyesha kutoridhishwa na wachezaji wa kigeni kutawala soka la Tanzania huku akiiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kukaa chini na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujadiliana namna bora ya kuzalisha wachezaji wazawa wenye ubora.

Kikwete ametoa kauli hiyo leo Juni 25 jijini hapa wakati akizungumza kwenye mbio za JKT Marathon zikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu jeshi hilo lianzishwe.

Alisema ni aibu kila siku mashabiki kuwataja wachezaji wa kigeni huku wazawa wakiwa hawapo.
“Ila bado mimi kilio changu tukazanie kuinua vipaji vya wachezaji wa ndani, Yanga na Simba, kila siku Mayele, Bangala, Diarra, Baleke, Chama, Ntibanzokiza sasa katika wale wanaosifiwa wachezaji wa Tanzania hawamo.

“Lakini sisi ukiuliza mchezaji gani maarufu Simba utasikia Baleke, utasikia kacheza mechi sita tu, Yanga kule utasikia Mayele sasa wakiondoka?

“Hili sio jambo dogo Mwinjuma (Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo) nilisema siku moja pale kwenye sherehe za Yanga mbona mnatoa wachezaji wengi, jibu lao TFF wakaongeza kutoka wanane wakapelekwa 12.

“Tunasukumwa na viongozi wa hizi klabu kubwa na tatizo lao ni kushinda tu, lakini nyinyi mliopo hapa hawa wanashinda lakini katika kushinda huko wachezaji wa Tanzania nao wanashinda?

Alisema hasemi kwamba wasichukue wachezaji kutoka nje ila wajiuliza kwanini wanaong’ara ni kutoka nje na wazawa hawafanyi vizuri.

“Lakini kama jukumu letu ni kushinda tu basi, mtu anasema kama unatafuta paka kwa kukamata panya una haja ya kuchagua rangi ya paka,” alisema Rais huyo Mstaafu.
Kuhusu riadha, Kikwete alisema watanzania wanapenda soka sana kuliko riadha lakini walioleta sifa kubwa nchini ni wanariadha na kutaka kupangwa kwa mikakati wa kufufua mchezo huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa alisema JKT itaendelea kudhamini na kuendeleza michezo na tayari timu ya wanawake ya JKT Queens imekuwa bingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) huku Mashujaa ikipanda Ligi Kuu.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda alisema jeshi litaendelea kudhamini na kuibua, vipaji vya wanamichezo nchini kwa manufaa ya jeshi na nchi kwa ujumla.
“Mchezo mwingine tunaojivunia katika Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) ni mpira wa miguu… tunatimu ya wanawake ambayo inaitwa JKT Queens, timu hii ndio bingwa wa timu zote wa Ligi Kuu kwa upande wa mpira wanawake imeshinda lakini kesho inaondoka kwenda kushiriki mashindano ya majeshi duniani,”alisema.
Mkuu wa Jeshi la JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele alisema lengo la mbio hizo ni kulitangaza jeshi hilo na kuweka hamasa katika jamii kupenda michezo.

Post a Comment

0 Comments