Header Ads Widget

Serikali Yaweka Pingamizi Tena Maombi ya Godbless Lema Kupewa Dhamana



Jana, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ilishindwa kusikiliza maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya kukata rufaa ya kupinga kuzuiwa kwa dhamana ya Lema. 


Mawakili wa Serikali waliomba muda wa kuwasilisha hoja za kupinga maombi hayo. 


Maombi hayo, yaliyotarajiwa kusikilizwa jana na Jaji Dk Modesta Opiyo yalikwama kutokana na kusudio la pingamizi lililowekwa na mawakili waandamizi wa Jamhuri katika shauri hilo, Paul Kadushi na Maternus Marandu.


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya Jaji Opiyo kuahirisha kusikiliza maombi hayo, Wakili wa Lema, Sheck Mfinanga alisema mawakili wa Serikali, wameomba wapewe muda kuwasilisha kiapo kinzani dhidi ya maombi hayo.


Alisema Jaji Opiyo alitumia busara kutoa uamuzi kuwa mawakili wa Jamhuri wawasilishe hoja hizo, Desemba 13 na upande wa utetezi utazijibu siku hiyo hiyo na uamuzi utatolewa Desemba 14, saa 6.00 mchana.


Jana Lema hakufika mahakamani, kwa kile kilichoelezwa kuchelewa kupelekewa hati ya kufikishwa mahakamani.


Lema anaendelea kushikiliwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupinga uamuzi wa hakimu mkazi, Desdery Kamugisha aliyempa dhamana Lema katika kesi namba 440 na 441/2016 ya kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.


Lema anatuhumiwa kuwa kati ya Oktoba 23 hadi 26, mwaka huu alitoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli katika maeneo tofauti katika mikutano yake ya hadhara.


Miongoni mwa kauli za Lema ni: “Nchi itaingia katika machafuko kama haitafuata misingi ya katiba na sheria na pia Rais Magufuli asipobadilika” 


Lema pia akiwa katika uwanja wa shule ya Sekondari Baraa alitoa kauli kuwa: “Kiburi cha Rais akiendeea kujiona yeye ni Mungu, hatafika 2020, Mungu atakuwa amechukua maisha yake, Rais ni mbabe…”

Post a Comment

0 Comments