Getrude Clement mwenye umri wa miaka 16 ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu anayesoma shule ya Sekondari Mnarani iliyopo jijini Mwanza, leo amepata nafasi ya kufika bungeni Dodoma baada ya kupewa mwaliko wa Serikali
Hivi karibuni Getrude alihutubia viongozi mbalimbali wa dunia kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa uliohusu mabadiliko ya tabia nchi uliofanyika New York Marekani ambapo leo Bungeni amewahimiza Watanzania kutunza mazingira na kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali na wataalamu wa mazingira ili kuyatunza mazingira wanamoishi.
Getrude amesema kuwa amefarijika kwa kuwawakilisha vijana wa Tanzania na dunia kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi ambapo mataifa 175 yalikutana kusaini makubaliano ya Paris.
Katika kuwahimiza vijana kujenga tabia ya kutunza mazingira, Getrude amewaasa vijana hasa wanafunzi kusimamia suala la utunzaji wa mazingira wakiwa shuleni kwa kwa kujiunga na klabu mbalimbali ambapo yeye amejiunga na klabu ya “Mali Hai” iliyopo shuleni anaposoma.
Kwa upande wa Watanzania kwa ujumla kwenye utunzaji wa mazingira, Getrude amesema kuwa ni vema wajifunze kutoka mataifa mengine yanavyosimamia utunzaji wa mazingira hasa matumizi ya mifuko ya plastiki.
Mwanafunzi huyo amekaribishwa na kutambulishwa kwa wabunge leo mjini Dodoma kwa heshima ya kuliwakilisha vema taifa wakati wa utiaji saini makubaliano ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki moon alimkaribisha Getrude kwa viongozi hao na kusema “Ni furaha yangu kumualika Getrude Clement ambaye pia ni mwakilishi wa vijana anayeishi Tanzania na anaziwakilisha sauti za vijana”.
0 Comments