RAIS Dk. John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 3,551, huku akiwanyima msamaha kwa mara ya kwanza wezi wa pikipiki, maarufu kama bodaboda na magari.
Kati ya wafungwa hao 3,551, Rais Magufuli amewaachia huru 580 na wengine 2,971 wamepunguzia moja ya sita ya vifungo vyao.
Rais alitoa msamaha huo jana wakati wa maazimisho ya miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali mstaafu Projest Rwegasira, ilisema wezi wa pikipiki na magari ni miongoni mwa waliokosa msamaha kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.
“Rais kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa msamaha kwa wafungwa 3,551 ambapo 2,971 watapunguziwa vifungo vyao kwa asilimia moja ya sita na 580 kuwachiwa huru,” ilisema taarifa hiyo.
Rais Magufuli alisema ni mategemeo ya Serikali kuwa wafungwa watakaoachiwa huru watarejea katika jamii kushirikiana na wenzao kujenga Taifa na watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.
Wafungwa walionufaika na msamaha huo, ni wale wenye ugonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu, saratani ambao wamethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Wilaya.
“Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini au zaidi, wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.
“Wengine walionufaika na msamaha ni wenye ulemavu wa mwili na akili ambao ulemavu huo umethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mganga Mkuu wa Wilaya,” ilisema taarifa hiyo.
Wafungwa ambao hawakuguswa na msamaha huo, ni wale waliohukumiwa kunyongwa, waliopewa adhabu ya kunyongwa na kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.
Wengine ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya (cocaine, heroin na bhangi), makosa ya rushwa, makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo.
Wengine ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.
Rais pia hakuwasamehe wanaotumikia kifungo kwa kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na ambao walitenda makosa hayo wakiwa na umri wa miaka 18, wale wenye makosa ya wizi wa magari na pikipiki, wanaotumikia kifungo chini ya sheria ya Bodi ya Parole na Sheria ya Huduma kwa Jamii.
“Waliokosa msamaha wengine ni wale waliotumia vibaya madaraka, waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.
“Wafungwa waliozuia watoto kupata masomo, wenye makosa ya utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu, kukutwa na viungo vya binadamu pamoja na vitendo vya mashambulizi na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino,” ilisema taarifa hiyo.
Hata hivyo, Rais Magufuli hakuwasamehe waliofungwa kwa makosa ya usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili, wizi ama ubadhirifu wa fedha za Serikali, makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi halali na wafungwa walioingia gerezani baada ya Februari 26 mwaka huu.
0 Comments