WANANCHI WAFANYA MAANDAMANO NA KUUA MBWA WALIOMUUA MWANAFUNZI NA KUMLA NYAMA.
. Waitaka serikali kumuondoa OCD kwa kushindwa kulinda raia na mali zao
.DC aagiza hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika
Na Bazil Makungu Ludewa na Nickson Mahundi
Wananchi wa Kata ya Ludewa Mkoa wa Iringa, wameungana na pamoja kufanya maandamano ya kushinikiza mbwa waliomuua mtoto na kumtafuna wauawe baada ya mmiliki wa mbwa hao kutishia kuwashtaki watakao husika kuwaua mbwa wake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa dharula ulioitishwa na Diwani wa kata ya Ludewa, Mama Monica Mchilo, walisema kuwa mbwa hao wamekuwa kero kubwa na tishio kwa muda mrefu kwa wananchi ambapo hadi sasa wameshateketeza mifugo mingi wakiwemo mbuzi lakini cha kushangaza kila wanapolipeleka suala hilo katika vyombo vya dola mmiliki huwaeleza walete ushahidi.
Kutokana na hali hiyo tata mkuu wa wilaya ya Ludewa, Juma Madaha, ameviagiza vyombo husika ikiwemo idara ya kilimo na mifugo, jeshi la polisi kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote anayehusika na tukio hili akiwemo mmiliki wa mbwa hao Bosco Thobias Lingalangala kwa sababu hakuna mtu aliye juu ya sheria.
Juhudi za kumpata mmiliki wa mbwa hao Lingalangala,(BOLI) ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa klabu ya yanga miaka ya nyuma hazikuzaa matunda kutokana na simu yake kutopokelewa na baadaye kuzimwa kabisa.
Hali hiyo imejitokeza tena kwa mmiliki wa mbwa hao alipoelezwa kuwa wamefanya mauaji na kumla mtoto wa darasa la tatu katika shule ya msingi Ludewa mjini aliyefahamika kwa jina la Ibrahim Chipungahelo (9).
Aidha mmiliki huyo aliwataka wananchi kuleta ushahidi licha ya kuwa Askari wa jeshi la polisi kwa kutumia silaha na kuuokoa mwili wa mtoto huyo ukiwa tayali umeshaliwa katika baadhi ya viungo.
Akiongea katika mkutano huo mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ludewa Bw.Omary Kiowi alisema tukio na kauli za mmiliki wa Mbwa hao wawili Bw.Bosco Lingalangala hazivumiliki kwa wanaludewa kwani amekuwa akiwatishia wananchi kwa kutumia bastola kila wakati hivyo kikao hicho kiliamuru mbwa hao wauawe na mmiliki achukuliwe hatua za kisheria.
“Tokea nizaliwe zijawahi kuona Mbwa akitafuna mtu, hii ni mara ya kwanza,hatuwezi kuvumilia na ninachokiomba wananchi msifanye fujo naamini tukitoka hapa kwa kushirikiana na ofisi ya mifugo pamoja na jeshi la Polisi tunakwenda kumuua mbwa aliyebaki na tunamtaka Bw.Bosco atushtaki wananchi wote na Serikali yetu kwa sababu anadhani yeye yuko juu ya sheria”,alisema Bw.Kiowi.
Kufuatia kauli za vitisho wananchi wakaomba kikao kiahirishwe na kuanza maandamano kuelekea katika nyamba ya mmiliki wa mbwa hao ambako aliuawa marehemu Ibrahim na kuhakikisha wananmuua mbwa aliyebaki kwa kupigwa risasi,kwa hasira walizo kuwa nazo wananchi hao waliamua kuondoka na Mbwa hao wote wawili wakiwa wamekufa na kupita nao mitaani huku wakiimba nyimbo mbalimbali.
Baada ya kuzunguka na mizoga ya mbwa hao mitaani kwa muda mrefu hatimaye walielekea katika ofisi ya kata na kuamua kuwachoma moto na kuwateketeza kabisa na kuendelea na kikao ambacho kiliibua shangwe na vifijo baada ya mzee Laurance Mtweve (Muhuchu) ambaye ni mzee mashuhuri kutoa kauli ya kuutaka uongozi wa kijiji kumuandikia barua mkuu wa wilaya ya Ludewa ya kufukuza Bosco kuishi eneo la Ikilu kutokana na vitisho vyake.
Mzee Muhuchu alisema kama uongozi wa wilaya utashindwa kufanya hivyo basi wazee wa wilaya ya Ludewa watamuandikia barua Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kuwa wamechoshwa na unyanyasaji wa Bw.Bosco hiyo hawamuhitaji wilayani hapa tena.
Alisema kwani imekuwa kawaida yake kuwatisha wananchi kwa kutumia bastola hali inayowafanya wananchi kuishi kwa kuhofia usalama wao kwani inaonekana yuko juu ya sheria kutokana na kufanya matukio ya ajabu lakini wanaoshtaki hupuuzwa na jeshi la polisi hapa Ludewa.
Aidha Diwani wa kata ya Ludewa kupitia CCM mama Monica Mchilo aliwataka wananchi kupunguza jazba wakati sheria inachukua mkondo wake ingawa awali alionesha kutoridhishwa na kauli za mmiliki wa mbwa hao kuwa atawashtaki watakaohusika kuwaua.
Mama Mchilo alisema hakuna aliyeridhishwa na kauli mbaya za Bosco lakini anaamini Serikali ni sikivu itasikia kilio cha wananchi wa kata ya Ludewa kutokana na vitisho vya mtu huyo ambaye hana hata chembe ya utu kwa kusema mbwa wasiuawe bali atawalipa fidia wafiwa.
Aliwashukuru wananchi kwa kufanya maandamano ya amani ambayo hayakuleta madhara kwa jamii lakini yalifanikisha kuwaua mbwa ambao walikuwa ni tishio kwa jamii hasa kwa wanafunzi wanaopita eneo hilo ambako aliwafugia mbwa hao.
Maziko ya mtoto Ibrahim
Wananchi wa Ludewa wakiwa katika maziko ya mtoto Ibrahim.
0 Comments